Salum Mayanga aenda ujerumani kuhudhuria kozi ya kimataifa ya ukocha
Posted on Mon 31st August 2009 8. 01PM by
WembasterMwalimu Salum Mayanga ameondoka nchini Jumamosi usiku kwa ndege ya KLM kwenda nchini Ujerumani kuhudhuria kozi ya kimataifa ya ukocha wa mpira wa miguu ‘International Coaching Course’ katika Kituo cha Michezo cha Hennef kilichopo karibu na jiji la Bonn.
Kozi hiyo ya wiki 3 inayoanza tarehe 31 August hadi Tarehe 18 September inahudhuriwa na makocha 24 wa mpira wa miguu kutoka nchi mbalimbali duniani na inaendeshwa na Chama cha Mpira cha Ujerumani (DFB).
Mwalimu Mayanga ambaye tangu aanze kuifundisha Mtibwa Sugar kama mwalimu mkuu katika msimu wa mwaka 2008/09 ameonyesha uwezo mkubwa na kuipatia timu mataji ikiwemo kombe la Tusker na Ngao ya Hisani; ana cheti cha ukocha cha ngazi pevu ‘advance diploma’ alichokipata kutokana na kozi iliyoendeshwa na FIFA.
Ni dhahiri kuwa mafunzo atakayopata Mwalimu Mayanga nchini Ujerumani yatamwongezea ujuzi na uwezo wa ufundishaji na hivyo kuihakikishia klabu ya Mtibwa mafanikio makubwa zaidi mbali ya kuwagawia ujuzi huo waalimu wenzake na kuwaendeleza wachezaji chipukizi ambao watakuja kuwa tegemeo kwa taifa hapo baadaye .
Katika kipindi atakachokuwa nchini Ujerumani, Mwalimu Mayanga ataikosa michezo mitatu ya Ligi ambayo timu ya Mtibwa itacheza. Michezo hiyo ni wa tarehe 4 Septemba ambapo Mtibwa itakuwa mgeni wa JKT katika Uwanja wa Uhuru, tarehe 9 Septemba dhidi ya Majimaji katika uwanja wa Majimaji na tarehe 19 Septemba dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Akiongea na www.mtibwasugar.com muda mfupi kabla ya kuondoka, Mwalimu Mayanga alisema: “sina hofu na kutokuwepo kwangu, naamini Mtibwa itaendelea kufanya vizuri kutokana na maandalizi mazuri tuliyofanya na programu ambazo tumekubaliana na wenzangu katika kipindi ambacho nitakuwa mafunzoni”.
Katika kipindi hicho timu ya Mtibwa itakuwa chini ya waalimu Mecky Maxime na Patrick Mwangata.
www.mtibwasugar.com inamtakia Mwalimu Mayanga safari njema na kozi yenye mafanikio.
Page 1 of 1