Mtibwa yaanza kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Manyema rangers
Posted on Mon 24th August 2009 7. 10AM by
WebmasterMabingwa wa Tusker na ngao ya hisani, timu ya Mtibwa Sugar, imeanza vyema ligi kuu msimu wa 2009/10 kwa kuifunga mabao 2-1 timu ya Manyema Rangers katika pambano lililochezwa jana Jumapili katika Uwanja wa Manungu, Turiani.
Mtibwa ambayo ilikamata nafasi ya tatu katika Ligi kuu ya Vodacom msimu uliopita na ambayo msimu huu imedhamiria kufanya vizuri zaidi ndiyo iliyotangulia kufunga mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Said Rashid, kwa shuti kali lillomshinda golikipa wa Manyema Oddo Nombo.
Katika mchezo huo, timu ya Manyema inayofundishwa na Kocha mzoefu nchini Abdallah ‘King’ Kibaden ambaye alikuwa kocha wa Mtibwa kwa msimu wa 2007/2008 na pia ikiwatumia wachezaji Oddo Nombo, Adam Matunga, Mussa Kipao, Amoah Zulu na Waziri Omari ambao waliwahi kuichezea Mtibwa kwa vipindi tofauti huko nyuma; iliweza kuonyesha kandanda safi na kutoa upinzani mkali kwa timu ya Mtibwa. Hata hivyo hadi mapumziko timu ya Mtibwa ilitoka uwanjani ikiongoza kwa bao moja.
Timu ya Manyema iliweza kusawazisha goli katika dakika ya 70 kupitia kwa mshambuliaji wake hatari Julius Mrope aliyepokea pasi kutoka kwa Mussa Kipao. Kupatikana kwa bao hilo kuliwaamsha vijana wa Mtibwa ambao waliongeza mashambulizi na kufanikiwa kupata bao la ushindi katika dakika ya 82 kupitia kwa nahodha wake Zuberi Katwila aliyepiga kona iliyoenda moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kutoka kwa wapenzi na washabiki wa Mtibwa waliofika kwa wingi kwenye uwanja wa Manungu .
Timu ya Manyema iliyopanda daraja msimu huu imethibittisha kuwa si timu ya kubeza ingawa haikuweza kufua dafu kwa vijana wa Mtibwa wenye uzoefu wa muda mrefu wa michuano ya ligi kuu.
Mtibwa inayofundishwa na Kocha Salum Mayanga aliyeichezea timu hiyo kuanzia mwaka 1988-1998 akisaidiwa na Mecky Maxime ambaye naye pia aliichezea Mtibwa kuanzia mwaka 1997-2009, wakisaidiana na Patrick Mwangata; watajitupa tena uwanjani siku ya Jumatano tarehe 26 kupambana na African Lyon ambayo katika mchezo wa kwanza ilitoka sare ya bao 1-1 na mabingwa watetezi Yanga. Pambano hilo litachezwa katika uwanja wa Uhuru.
Katika michezo michezo mingine iliyochezwa jana ambayo ilikuwa ndiyo siku ya ufunguzi wa pazia la ligi kuu msimu wa 2009/10, timu ya Prisons ililala nyumbani 2-1 kwa JKT Ruvu, Toto African ilitoka sare ya 2-2 dhidi ya Moro United katika Uwanja wa Kirumba, Kagera
Sugar ilitumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuilaza mabao 3-2 timu ya Azam FC, Majimaji ilikubali kipigo cha mabo 2-0 nyumbani dhidi ya Simba nao mabingwa watetezi Yanga wakatoka sare ya 1-1 dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu, African Lyon.
Wachezaji katika mchezo wa jana walikuwa kama ifuatavyo:
MTIBWA: Shaaban Kado, Obadia Mungusa, Idrissa Rajab, Chacha Marwa, Shaaban Aboma, Zubeir Katwila, Said Mkopi/Zahoro Pazi, Abdulhalim Humoud, Pius Kisambale, Said Rashid/Hussein Javu, David Mwantobe/Soud Abdallah
MANYEMA: Oddo Nombo, Sixbert Moh’d, Yussuf Nguya, Menard Mgaya, Humoud Thabit, Amoah Zulu, Julius Mrope, Adam Matunga, Mussa Kipao, Ally Alawy/Benedict Ngassa, Waziri Omary/Ally Mohammed.
Wakati huohuo kwa mujibu wa Gazeti la mwananchi toleo la leo, MABINGWA watetezi Yanga wameanza ligi kwa kusuasua baada ya kulazimishwa sare 1-1 na African Lyon, huku watani wao Simba wakitoka kifua mbele 2-0 dhidi ya Majimaji ya Songea.
African Lyon iliyopanda daraja msimu huu iliutawala vizuri mchezo huo dhidi ya mabingwa hao katika kipindi cha kwanza na kupoteza nafasi nyingi za wazi, pamoja na kushindwa kutumia kona tano walizopata katika dakika 15 za mwanzo.
Chipukizi wawili ndugu Mohamed na Mbwana Samata walionekana kuinyanyasa ngome ya Yanga na walikosa mabao katika dakika 3, 27 kwa mashuti yao kuokolewa na kipa Obran Cuckovic aliyekuwa shujaa kwa mabingwa hao.
Kipindi cha pili Yanga walijirekebisha na kupata bao kupitia kwa mshambuliaji Jerryson Tegete akimalizia vizuri krosi ya Amir Maftah.
Kuingia kwa bao hilo kuifanya Lyon kuongeza mashambulizi na kufanikiwa kupata penalti dakika 71, baada ya Nsajigwa kuwangusha Mbwana kwenye eneo la hatari, lakini kiungo Rashid Gumbo alikosa.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania alijirekebisha na kufunga bao la kusawazishia kwa Lyon dakika 88 akipokea pasi nzuri ya John Nguya.
Mashabiki wa Yanga walioanza kurusha chupa za maji uwanjani wakimlenga mshika kibendera Hamis Changwalu na kusababisha mchezo huo kusimama kwa dakika tatu, hali iliyopelekea waamuzi hao kulolewa nje ya uwanja na ulinzi mkali wa polisi Uwanja wa Uhuru mwisho.
Kutoka mjini Songea, Joyce Joliga anaripoti; wenyeji Majimaji wamekubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba katika uwanja wa Majimaji.
Vijana hao wa Msimbazi waliosahau matatizo yote ya nje ya uwanja yanayoikabili, kwa kupata bao la mapema dakika ya 3 lililofungwa na Mohamed Banka baada ya ushirikiano mzuri kati ya Mussa Mgosi na Emmanuel Okwi ambaye alimpa pasi mfungaji.
Hadi mapumziko Simba ilikuwa ikiongoza kwa bao 1- 0 ilicheza vizuri katika dakika za mwanzo, lakini mchezo ulibadilika na kuwa wa kushambuliana mara baada ya kupata bao.
Katika mechi hiyo Simba ilikuwa ikiwatumia Danny Mrwanda na Mussa Mgosi katika winga za pembeni kufanya mshambulizi yake.
Simba inayofundishwa na kocha Patrick Phiri iliweza kupata bao la pili katika dakika ya 54 kupitia mshambuliaji wake hatari Danny Mrwanda.
Kutoka Mbeya, Blandina Nelson anaripoti, kwenye Uwanja wa Sokoine, Wenyeji Tanzania Prisons wameanza vibaya ligi kwa kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa JKT Ruvu.
JKT Ruvu imepata bao lake la kwanza dakika ya tatu kupitia Hussein Bunu aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Bakari Kondo.
Katika Kipindi cha pili dakika ya 57, Prisons ilisawazisha bao kufuatia penalti iliyopigwa na Seleman Msengi baada ya mlinzi wa JKT Ruvu kumchezea vibaya mchezaji wa Prisons.
Mchezaji wa JKT Ruvu, Kess Mapunda alipewa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya Benjamin Asukile katika mechi hiyo.
JKT Ruvu iliandika bao la pili, kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Mapunda dakika ya 90 na kusababisha vurugu uwanjani hao.
Uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba,Kagera Sugar iliwakaribisha Azam, wageni hao walikuwa wa kwanza kupata bao dakika 8 kupitia kwa John Boko, lakini dakika ya 36, Paul Kabange wa Kagera Sugar alisawazisha bao hilo kabla ya mshambuliaji Mike Katende hajafunga bao la pili.
John Boko alifunga bao lake la pili kwa Azam, matokeo yakifikiria kuwa ni sare wenyeji Kagera Sugar iliandika bao la tatu na kujipatia pointi tatu muhimu siku ya ufunguzi.
Timu ya Toto African iliikaribisha Moro United katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Toto iliyo chini ya kocha Mbwana Mataka ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza.
Katika kipindi cha pili, Juma abdalah wa Moro United alisawazisha bao hilo katika dakika ya 54.
Dakika ya 64, Jacob Masawe aliiandikia Toto African bao la pili kabla ya vijana wa Moro United wanaofundishwa na Juma Mwambusi haijasawazisha
Page 1 of 1