KADO aliyetimiza ndoto zake Mtibwa Suga kwa kutwaa Tusker Cup, kuliwania tena mwaka huu
Posted on Thu 1st January 1970 2. 00AM by
Number10 Magazine toleo la 4
“NILIKUWA na ndoto ya kutimiza muda mrefu, jambo lililokuwa likiiumiza kichwa timu yangu kwa muda mrefu na kwa bahati nzuri imetimia”
Kabla ‘hajatoka’ alikuwa mfuasi mkubwa wa kipa mwenzake Juma Kaseja, na hatimaye leo hii anacheza naye uwanja mmoja.
Kwa umbo ni mfupi, ana mwili wa wastani lakini ana uwezo wa kujipinda kuelekea pande zote mbili za milingoti ya magoli.
Anaitwa Shaban Hassan Shaban anafahamika zaidi kama Shaban Kado, alizaliwa miaka 19 iliyopita na ni kipa wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, mabingwa wa michuano ya Tusker.
Katika michuano hiyo iliyochezwa jijini Dar es Salaam Desemba mwaka jana, Kado alionyesha umahiri mkubwa langoni na kuweza kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa.
Awali Mtibwa ilionekana kama timu sindikizi lakini upepo ulikuja kubadilika na kuonekana moja kati ya timu zilizodhamiria kutwaa ubingwa.
“Kwa miaka mingi Mtibwa ilikuwa ikikosa kuchukua ubingwa wa Tusker, nikajiuliza tatizo lipo wapi?, njia pekee ya kuisaidia timu yangu ilikuwa ni kujituma langoni,” anasema Kado.
Alifungwa mabao mawili tu katika mechi nne alizocheza katika michuano ya Tusker huku timu yake ikifunga mabao manne.
“Najipongeza kwa kufungwa mabao machache, lakini nawashukuru mabeki wangu kwani waliweza kufuata vyema maelekezo yangu na kuweza kutoruhusu kuharibikiwa,” anasema Kado.
Anasema alifurahi zaidi walipoifunga Yanga bao 1-0 katika mchezo wa mwisho wa kundi A katika michuano hiyo licha ya awali kufungwa na timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) kwa bao 1-0.
Kutokana na ushindi huo, ilipigwa kura kati ya timu hizo tatu (Yanga, URA na Mtibwa) na Yanga kutupwa nje ya michuano(zote zilikuwa na pointi sawa). Mtibwa ilicheza nusu fainali na Tusker ya Kenya na kuifunga mabao 2-1.
“Tusker ni bora zaidi ya Yanga, wana kasi ya mpira pia wanapanga mashambulizi ya hatari zaidi lakini kutokana na kujidhatiti kwetu tuliweza kuwafunga mabao 2-1,” anasema Kado.
Katika mchezo wa fainali, Mtibwa iliifunga URA bao 1-0, na kufungua ukurasa mpya wa mafanikio yake katika miaka hii ya 2000.
Kado anamtaja Iker Casilas kama kipa bora duniani na anayefaa kuigwa na kipa yeyote, pia anamkumbuka sana Compos wa Mexico kutokana na umahiri wake langoni.
Kado anasema hawakuifunga Yanga kwa nguvu ya soda katika michuano ya Tusker japokuwa Mtibwa imefungwa mara mbili na Wanajangwani hao katika michezo miwili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Nakubali kwamba wanatufunga (Yanga) katika Ligi, lakini hebu angalia ni idadi ya mabao mangapi wanayotufunga utaona ni 1-0 kila mara, bado Mtibwa ni imara,” anasema Kado.
MFUPI ANADAKAJE?
“Ufupi si tatizo katika soka, kwani wapo na walikuwapo makipa wengi wafupi walioweza kudaka kwa ustadi mkubwa,” anasema Kado huku akitolea mfano kwa Kaseja na Compos.
Anasema kinachotakiwa ni kipaji cha kipa na utashi pamoja na moyo wa kujituma awapo langoni.
KADO MWANAMUZIKI:
Ni jambo la kawaida kumkuta binadamu akiwa amezaliwa na vipaji viwili, mbali ya u-kipa wake, Kado aliwahi kutengeza baadhi ya vionjo katika ala za nyimbo moja ya Ali Kiba.
Kazi hiyo ya muziki aliwahi kuifanya katika Studio ya Beyon Records ya Mabibo External na hata mtaani anapoishi rafiki zake wakubwa ni Ali Kiba na Madee.
BAADAE:
“Nina malengo mengi katika maisha yangu ya soka, nawaza kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na tayari kuna mipango nimeanza kuifanya,” anasema Kado.
Ana ‘contact’ na watu wake waliopo Norway na Afrika Kusini ili apate nafasi ya kucheza huko.
Kado anasema safu ya ushambuliaji ya Simba ni kali kuliko zote katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu lakini bila kuwahusisha Emeh Izuchukwu na Orji Obinna.
ALIKOPITA:
Alianza kucheza soka mwaka 1999 katika timu ya Yetu Afrika kisha akajiunga na Magereza Dodoma mwaka 2000 na mwaka mmoja baadae alirudi tena katika klabu yake ya awali.
Mwaka 2003 alijiunga na Sifa United ya Mabibo na mwaka mmoja baadae alijiunga na Mabibo United, baada ya kipaji chake kuonekana alisajiliwa na Moro United mwaka 2006.
Kabla ya kusajiliwa Moro United, Kado alitoswa katika majaribio yake aliyofanya katika timu hiyo mwaka 2005 na kujiunga na Rhino ya Morogoro ndani ya mwaka huohuo.
Baada ya kufanya vyema na Rhino, meneja wa Moro United, Willy Marekano alimuita na kumpa fomu za timu yake ili asaini kucheza kwa msimu wa 2006/07.
Alisajiliwa na Mtibwa mwaka jana baada ya kutokea hali ya kutoelewana na viongozi wa Moro United. Na hadi sasa ni miongoni mwa wachezaji tegemezi wa Kocha Salum Mayanga.
Mwisho
Previous articlesPage 1 of 4    
[Next article]    
[Last article]